Home Hadithi/ Makala Siwezi kumuacha mume wangu ingawa ana VVU.:soma makala hii ya kusisimua.

Siwezi kumuacha mume wangu ingawa ana VVU.:soma makala hii ya kusisimua.

10 min read
0
0

“NIMEMPOKEA na kumkubali bila kujali hali yake, nimemuuguza akiwa kwenye hali mbaya hadi sasa bado nampenda mume wangu japo nimeshauriwa sana niachane nae lakini sipo tayari.
“Kuugua ukimwi si kufa… unaweza ukafa kwa malaria, unaweza kufia usingizini, najua ningekuwa mimi ndiyo nina ukimwi asingekubali kuendelea kuishi na mimi, angeniacha, ni moyo tu.”
Hayo ni maneno ya mke wa Mashauri Charles (jina tunalihifadhi), mkazi wa Bukombe anayekiri anaishi na mume muathirika wa virusi vya ukimwi (VVU) anayetumia dawa za kufifisha makali ya maradhi hayo.
Kwa upande wake Mashauri anakiri kwamba ingekuwa mke wake huyo kama ndiye mwenye maambukizi ya ukimwi asingekubali kuishi naye, angemfukuza.
Mashauri (37) ni baba wa watoto wanne ambao hawajaathirika na VVU. Anaishi na mke wake kwa miaka 11 sasa bila kumwambukiza licha ya kushiriki naye tendo la ndoa kabla na baada ya kugundulika. Mtoto mdogo wa Mashauri ana miaka tisa.
Mwanamke huyo ambaye hakutaka jina wala picha yake vichapishwe gazetini akihofia familia yake kumtenga kwa kuwa anaishi na mume mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, anasema japo hana lakini anaamini kwamba ukimwi si kifo.
Anasema baada ya kugundulika kwamba mumewe anaishi na VVU wakati huo ameshaanza kushambuliwa na maradhi nyemelezi, alikosa raha akiamini hata yeye atakuwa mgonjwa, hivyo ilimuwia vigumu kuikubali hali hiyo.
“Alikuwa anaumwa sana bila sisi kujua kama ameathirika, tulihangaika kwa waganga, huko akipata nafuu kidogo, kisha anarudia tena kwenye hali yake.
“Tulikubaliana twende hospitali baada ya kuhangaika huko kwingine, tukaenda hospitali ya Ushirombo tukapata vipimo, mwenzangu akaonekana anao huu ugonjwa, akaogopa, alijua nitamwacha (kicheko).
“Mwanzo sikutaka kupima, nilijua nami ninao lakini wahudumu wa hapa walinishauri nikapima… kwa kweli sikuamini kama sina maambukizi,” anasema mke wa Mashauri huku akieleza kwamba hiyo ilikuwa mwaka 2002.
Anasisitiza kwamba tangu wakati huo hadi Juni mwaka huu ameshapima mara tisa, hana maambukizi. Anasema wanao watoto wawili ambao nao hawana maambukizi hivyo anaishi kwa furaha na mumewe.
“Sikupenda kumuacha mume wangu kwa sababu si vizuri kumnyanyapaa mwenye ugonjwa huu, tena ninaishi naye hata familia yangu haijui kama mwenzangu yupo kwenye hali hii.
“Wazazi wangu walimfukuza mke wa kaka yangu baada ya kugundulika naye anaumwa ukimwi, walimfukuza kwa kumtupia virago nje bila kaka yangu kwenda kupima.
“Nilijua ningeishirikisha familia yangu katika hili ningetengwa au ningelazimishwa kuachana na mume wangu wakati bado nampenda hata kama anaishi na ugonjwa huu,” anasisitiza mke wa Mashauri.
Historia ya Ugonjwa
Mashauri anasema kabla ya kupata maambukizi ya VVU alikuwa akifanya kazi kwenye Kampuni ya Kihispania iitwayo ABD iliyopewa kazi ya kusambaza umeme wilayani Bunda, Mara.
Kwa mujibu wa Mashauri ambaye kwa sasa anafanya kazi ya kuwahamasisha wananchi kupima kwa hiari na kujikubali, anasema akiwa anafanya kazi huko alikuwa na fedha za kutosha alizozitumia kutoka na wanawake tofauti.
“Nikiwa kwenye ile kampuni ukweli nilikuwa napata pesa nyingi… sikutulia kwa kweli, nilikuwa naishi na mke mwingine, nikaachana naye kwa sababu ya kurukaruka.
“Nilipokutana na mama huyu akanituliza lakini bahati mbaya nilikuwa nimeshapata maradhi haya… hatukuishi kwa raha sana magonjwa kila siku.
“Hadi tunakwenda kupima mwaka 2002 nilikuwa na CD4 27, yaani nilidhohofika sana…nilihofia kusema pengine mama huyu atanikimbia, lakini alinipenda hadi sasa namshukuru hakuninyanyapaa.
“Nilianza kunywa dawa za ARV mwaka 2007 wakati wote huo mke wangu alikuwa ananihudumia kwa vyakula na dawa za kutuliza maumivu, kwa sababu wakati huo dawa zilikuwa hazipatikani huku kwetu,” anasema Mashauri mwenye watoto wanne.
Licha ya kuishi na maradhi hayo kwa miaka 11 Mashauri anasema kitendo cha mke wake kuendelea kuishi naye kwa uaminifu kinamfanya ajione sawa katika jamii na kumpa nguvu ya kujikubali.
Hivi sasa CD4 za Mashauri zimeongezeka na kufikia 799, hasa baada ya kuanza kunywa dawa za ARV anazopata kutoka kwenye Kliniki ya Tiba na Matunzo iliyopo kwenye Hospitali ya Bukombe kwa msaada wa Shirika la AGPAHI.
“Ninajitolea kila wiki nafika hapa hospitali mara tatu kwa ajili ya kukutana na waathirika, nawaeleza namna ya kujikubali na wengine nawashawishi wapime VVU, huwa nawaambia mfano wangu.
“Unyanyapaa ni tatizo katika jamii linaloanzia kwa mgonjwa mwenyewe… huwa naenda kwenye matamasha mbalimbali kuwahamasisha wanajamii waache unyanyapaa,” anasema Mashauri ambaye sasa ni mkulima na mfugaji.
Anakula nini?
Anasema anakula mboga nyingi za majani na vyakula vingine huku akisisitiza kwamba anazingatia ushauri wa madaktari.
“Kabla sijaanza dawa mke wangu alikuwa akinikazania sana kula mboga za majani zilizochemshwa tu hasa mchicha. Nilikuwa nakula vyakula vya wanga pia.
“Ugali wa dona samaki wabichi na nyama kidogo lakini kila siku nilikuwa nahakikikisha nakula mboga nyingi za aina mbalimbali za majani,” anasema huku akitabasamu.
Mke wake anaongeza kwamba aliambiwa kwamba chakula anachopika kwa ajili ya familia ndicho alichokuwa akimpa mgonjwa.
“Nilikuwa nachukua mboga aina tofauti za majani nachemsha pamoja nampa anakula kila wakati ila unapofika muda wa kula tunakaa pamoja na watoto wetu,” anasema.
Daktari anasemaje?
Mwandishi wa makala hii alizungumza na wataalamu mbalimbali wa afya wanaosema inawezekana wanandoa wakaishi kwa mmoja kuwa na maambukizi ya VVU mwingine kutokuwa nayo.
Mratibu wa kiliniki ya tiba na mafunzo ya Bukombe, Dk. Honoratha Rwezahura, anasema kitaalamu wanandoa hao wanaitwa ‘Discondac couple’ huku akibainisha kwamba inategemea na kinga za mwili za mmoja wao.
“Mtu mwingine maumbile yake kiphisiolojia anashindwa kutengeneza ‘antibodies’ ambazo tunazipima ili kugundua kama ameathirika ama la.
“Inawezekana kabisa kwa aliyeathirika asimwambukize mwingine kwa sababu kinga zake za mwili (CD4) zipo juu hivyo virusi vinakosa nguvu.
“Kama ni mwanamume anaweza kumtia mimba mke wake bila kumwambukiza VVU na wakapata mtoto aliye salama… mtu anayetumia ARV virusi vyake havizaliani tena mtu huyo ukimpima unaweza kukuta hana virusi,” anasema Dk. Honoratha.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, virusi vikipewa dawa vinajificha kwenye matezi, ndiyo maana wataalamu wanashauri mtu apime mara tatu kwa vipindi tofauti.
Anasema virusi vikizoea dawa vinakosa nguvu ya kuzishambulia CD4, ndiyo maana wanawashauri wagonjwa kutumia dawa hizo siku zote za maisha yao.
Facebook Comments

Load More Related Articles
Load More By Osward Anderson
Load More In Hadithi/ Makala

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Yanga kukosa wachezaji hawa dhidi ya Simba

Yanga imethibitisha itawakosa wachezaji wake watatu katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya…